Barbro Johansson ni shule inayomsaidia mwanafunzi kufikia uwezo wake wa juu kitaaluma
Hakuna kitu kinachompa furaha mzazi kama kuona mwanaye anafanya vizuri kitaaluma. Ndiyo, nimetaja taaluma kwa sababu ndiyo urithi pekee wenye thamani katika maisha ya mtoto.
Hakuna kitu kinachompa furaha mzazi kama kuona mwanaye anafanya vizuri kitaaluma. Ndiyo, nimetaja taaluma kwa sababu ndiyo urithi pekee wenye thamani katika maisha ya mtoto.
Kufanya vizuri kwa mtoto kitaaluma hakutokei kama miujiza bali huja kutokana na uwekezaji ambao mzazi anatakiwa kuufanya.
Uwekezaji huo unahusisha fedha, muda na rasilimali nyingine.Pia uwekezaji huu unahusisha kumchagulia mtoto shule bora ambayo itakuwa chanzo cha yeye kufanya vizuri na kufikia malengo yake.
Shule ya sekondari ya wasichana ya Barbro Johansson iliyoko Luguruni kata ya Kwembe, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, inatimiza ndoto za wazazi wengi wenye malengo ya watoto wao kufanya vizuri kitaaluma.
Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye shule hiyo, imeshuhudiwa ikifanya vizuri kwenye mitihani mbalimbali ya Taifa, jambo linaloifanya kuwa chaguo namba moja kwa wazazi kuwapelekea watoto wao.
Gazeti hili lilifika kwenye shule hiyo na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shule hiyo , Halima Kamote ambaye pamoja na mambo mengine alieleza namna ambavyo wamejizatiti katika kumuandaa mtoto kitaaluma na kinidhamu ili kumwezesha kukabiliana na mazingira na kutatua changamoto katika jamii yake.
“Shule ya Barbro ni shule ya sekondari ya wasichana ya bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita iliyoanzishwa mwaka 2000 eneo la Ada Estate, Kinondoni, Dar es Salaam, ikiwa na darasa anzilishi la kidato cha kwanza lililokuwa na wasichana 40 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, wote wakati huo wakisoma kwa ufadhili wa asilimia 100,” anasema Halima.
Anasema wanafunzi wanaopokelewa kwenye shule hiyo ni wasichana kutoka katika familia zote, wale wanaolipa na wapo pia wanaotoka kwenye familia zenye kipato duni ambao husoma kwa ufadhili; hawa ni asilimia 7 mpaka 10 ya wanafunzi wote.
“Wanafunzi wetu wanafanya vizuri kitaaluma ingawa hatuwachuji kutokana na ufaulu darasani bali sera yetu ni kumsaidia mwanafunzi kufikia uwezo wake wa juu (maximum potential) katika taaluma, hivyo kufanya vizuri katika masomo. Hili linafikiwa kupitia mbinu mbalimbali tunazozitumia kama vile kuwafundisha katika mazingira rafiki. Pia nidhamu chanya isiyokuwa na matumizi ya viboko, ushauri na unasihi kwa wanafunzi, kuwajengea hali ya kujiamini kupitia programu za wasemaji wa wiki, malumbano ya hoja, ushirikishwaji wa wazazi katika maendeleo ya wanafunzi kupitia kweny Umoja wa Walimu na Wazazi (PTA) na kuwapa mafunzo ya ziada kwa wale walioshindwa kufikia ufaulu mzuri (remedial classes),” anasema Halima
Halima anasema shule hiyo inajulikana kwa kutoa wanafunzi tofauti na wanakuwa wamejengewa misingi imara ya kujiamini, kujitegemea, kutetea yale ambayo yana manufaa kwao na kwa jamii na hivyo kutengeneza viongozi bora.
“Sisi ni shule ya sekondari, wanafunzi wanaelekezwa na kushauriwa kusoma masomo wanayoyaweza na ambayo wanapenda katika sayansi, biashara au Sanaa,” anasema Halima.
Anaongeza kuwa wanapofika kidato cha nne wanapewa semina ya uchaguzi wa tahsusi (Combination) ili kuwafikisha kwenye ndoto zao kwa mfano; PCB kwa madaktari, PCM kwa wahandisi, ECA kwa watu wa uchumi, HKL kwa wanasheria nk.
Anasema mwanafunzi anahimizwa kufanya vyema kwenye masomo yake huku akijua fika anataka kuwa nani maishani. Hivyo akifika kidato cha tano uchaguzi wa tahsusi unazingatia utashi wake wa kazi maishani pamoja na uwezo wake kitaaluma katika masomo husika. Zaidi ya yote kupitia kwenye klabu zao wanafunzi wanafundishwa ujasiriamali, sanaa za mikono na ubunifu ambazo pia huwasaidia maishani kama ajira aidha za kipato cha pembeni au kama kazi za kujiajiri.
“Tunayo maabara ya compyuta iliyosheheni kompyuta za kisasa na Wi-Fi kwa ajili ya mtandao. Wanafunzi wanaitumia maabara hiyo kwa kujifunza somo la kompyuta lakini pia kwa kupata taarifa za masomo (materials) mbalimbali,” anasema Halima.Pia CD zinazotumika kuwafundisha wanafunzi baadhi ya mada ngumu ili waelewe vizuri mchakato wa kutengeneza mayai ya viumbe hai(meiosis) na ule wa kugawanyika kwa chembechembe za uhai (Mitosis) ni ngumu kuzielezea kwa kufikirisha lakini hizi programu saidizi (simulation programmes) zinamfanya mtoto aelewe vizuri.
Kuhusu nafasi ya shule hiyo katika kuwafanya wanawake kupenda sayansi Halima anasema “wanawake wengi wanafikiri masomo ya sayansi ni magumu kwa sababu ya kufikirishwa na watu tu. Tunachofanya ni kuwatia moyo na kuhakikisha wanafundishwa kuelewa na hatimaye kufanya vizuri katika masomo hayo.”
Anasema “maabara za Kemia, Biologia, Fizikia zote zimesheheni vifaa na kemikali kwa ajili ya majaribio ya kisayansi, “Barbro sera yetu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anaelewa, hatujali tunarudia mara ngapi masomo kwa vitendo katika maabara hadi mwanafunzi aelewe kwa kufanya mwenyewe,” anasema Halima.
Kuhusu ushirikiano na serikali na wadau wengine Halima anasema wanafanya kazi karibu na Serikali na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha wanatoa elimu bora. “Serikali ya Sweden ilitoa msaada mkubwa katika kipindi cha miaka 12 katika ujenzi wa shule hii. Serikali nayo ilitupa usajili, tunakaguliwa na wadhibiti ubora, tumepatiwa huduma za maji umeme, barabara na tunafanya mitihani ya Taifa,” anasema Halima.
Anasema rafiki zetu wanaendelea kutupa msaada wa kusomesha watoto wanaotokea katika mazingira magumu. Wazazi wa wanafunzi wa shule ya Barbro wamekuwa wadau wazuri wa maendeleo ya elimu ya wasichana wao hapa shuleni.
Akizungumzia mikakati ya shule hiyo Halima amesema wana mpango wa kuanzisha shule ya wavulana hapo baadaye. Tayari wana ardhi karibu na shule hiyo ya wasichana kwa ajili ya kufanya ujenzi huo.
Kuhusu mafanikio ya shule hiyo Halima anasema “Barbro Johansson imesimama kwa miaka 21 sasa ikitoa wahitimu 2844 ambapo asilimia 99.9 ya wanafunzi wote walifaulu na kuendelea na ngazi nyingine za elimu. Katika kipindi chote wamepata mafanikio makubwa kitaaluma. Shule imetoa wanafunzi bora (Best top 10) katika masomo mbalimbali yakiwemo kompyuta, Hisabati, Kemia, Jografia na Kifaransa.
Anasema wanafunzi wao wameshinda kimataifa na kitaifa katika malumbano ya hoja (debate) na kuzungumza mbele za watu (public speaking). Pia wameleta ushindi katika michezo, Sanaa na tuzo mbalimbali kama vyeti, vikombe na ngao nyingi tulizonazo zinavyoonyesha.
Kuhusu changamoto wanazokutana nazo Halima anasema, changamoto zilizopo hasa ni kuhusiana na fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa majengo na miundombinu. Fedha za ufadhili wa wanafunzi wanaotokea kwenye familia zenye kipato duni zimepungua mno kiasi cha kupunguza idadi ya wanafunzi hao shuleni pamoja na uhitaji mkubwa.
“Miaka 10 ijayo shule itakuwa zaidi kufikia wanafunzi 800 na tutakuwa na shule ya wavulana zote mbili zikisaidia kukuza elimu ya mtoto wa kitanzania,” anasema Halima.
Unaweza kuwasiliana na shule ya Barbro Johansson kwa kutembelea tovuti ya www.johatrust.ac.tz au kupiga simu +255 222 926 482 na +255 757 063 349.